SIMULIZI|BOSS - SEHEMU YA KWANZA.

  


              SEHEMU YA KWANZA

Aisha alikuwa amehitimu kwa heshima kutoka chuo kikuu kimoja cha kifahari nchini. Alikuwa amefanya kazi kwa kusoma kwa bidii miaka yote ya masomo yake, akiamini kuwa elimu ilikuwa ufunguo wa maisha bora. Alikuwa na ndoto kubwa za kupata kazi nzuri katika kampuni kubwa na kuweza kuwasaidia wazazi wake ambao walikuwa wamejitahidi sana kumfikisha hapo alipo.

Siku aliyopewa cheti chake, furaha ilikuwa imejaa usoni mwake. Aliwaza kuhusu maisha mapya ambayo yangeanza mara tu atakapopata kazi. Alijua kwamba kupata kazi kungekuwa changamoto, lakini alikuwa na uhakika kwamba kwa sifa zake zote, angepata kazi haraka.

Wiki zilipita, kisha miezi. Aisha alikuwa akituma maombi ya kazi kila mahali, lakini hakuna hata mmoja aliyempa majibu mazuri. Alikuwa akipiga simu kila siku, akifuatilia maombi yake, lakini majibu yake yalikuwa ni yale yale: "Tutakupa taarifa."

Aisha alianza kuhisi kukata tamaa. Alikuwa amechoka kukaa nyumbani bila kufanya chochote. Alikuwa amezoea maisha ya shule, ambapo alikuwa na ratiba ya kila siku na malengo ya kufikia. Sasa, alikuwa akisikia kama maisha yake hayana maana.

Wazazi wake walijaribu kumfariji, lakini Aisha alijua kwamba walikuwa wakihisi vibaya vile vile. Walikuwa wamewekeza sana katika elimu yake, na sasa walikuwa wakiona kwamba uwekezaji wao ulikuwa ulikwenda bure.

Aisha aliamua kuchukua kazi yoyote ile aliyopata, hata kama haikuwa kazi aliyokuwa ameisoma. Alifanya kazi kama msaidizi wa ofisi, katika ofisi za kata zilizopo mtaani kwao lakini mshahara ulikuwa mdogo sana, mshahara ambao ulikua ukitolewa kama posho kwa siku na Mkuu wa wilaya yao kwa wafanyakazi wote waliojitolea na kazi ilikuwa ngumu. Alihisi kama alikuwa amepoteza miaka yote aliyoisomea.

Katika kipindi hiki kigumu, Aisha alijifunza mengi kuhusu maisha. Alijifunza kuwa maisha hayana uhakika, na kwamba hata watu wenye elimu wanaweza kupitia nyakati ngumu. Alijifunza pia kuwa ni muhimu kuwa na subira na kuendelea kujaribu, hata wakati mambo yanaonekana kuwa magumu.

Aisha aliendelea kutuma maombi ya kazi, na hatimaye, baada ya miezi kadhaa, alipata kazi katika kampuni ndogo. Mshahara ulikuwa mdogo pia, lakini alikuwa na furaha sana kwani alikua katika njia ya ajira tofauti na mwanzo alipokuwa ilikua ni kujitolea na kupata uzoefu. Alikuwa amepata fursa ya kuanza tena maisha yake.

Alifata taratibu zote za kukabidhi ofisi kwa mtendaji wa ofisi ya kata,alifanikiwa na alipata baraka zote kutoka kwao ikafanyika sherehe fupi ya kumuaga kutokana na namna alivyoishi pale ofisini na uchapakazi wake uliotukuka,hakika ilifana na alifurahi pamoja na familia yake ambayo ilitambua mchango wake kwao.

Baada ya siku kadhaa alipata barua ya kuhitajika kazini na haikumhitaji yeye kufanyiwa usaili,alipita moja kwenye majukumu ya kazi ambayo hii ndio hasa aliisomea.Siku ya tatu baada ya kupokea ujumbe ule ndio ilikua awe amefika Ofisini.Usiku wa kuamkia kazini ulikua mrefu zaidi ya siku yoyote maishani mwake,kila akilala alijikuta akiamka kuangalia labda pameshakucha ,Lakini haikua hivyo.

Jumatatu ya Novemba Mosi,ilikua imeshatimu saa moja na nusu asubuhi,uso wa Aisha ulikua ukitazamana na msichana mmoja mrembo aliyepo mapokezi,mkono wake ulikua bize kuandika taarifa zote alizozipata kutoka kwa Mwajiriwa mpya wa kampuni Ile ya Kutengeneza nguo za Watoto na wanawake huku kwa kiasi kidogo nguo za ndani za kiume zilikua sehemu moja wapo katika Kampuni hii,nazo zilitengenezwa.

Baada ya hapo Aisha alifata maelekezo yote anayopewa na Secretary yule pale mapokezi.

"Nyoosha moja kwa moja kufuata korido hiyo mbele yako,mkono wa kushoto mlango wakwanza unapaswa kuingia kuonana na Bosi" Maelekezo kutoka kwa Secretary akiyatoa kwenda kwa Aisha.

Maelekezo hayo aliyasikia vyema Lakini alikua na hofu hukuakitumia kitambaa chake laini kufuta kijasho chembamba kinachomtoka.Aliongoza moja kwa moja kufuata korido aliyoelekezwa.

"Ingia"

Sauti kutoka ndani ilimkaribisha Aisha baada ya kugonga mlango kupiga hodi.Aisha anafungua mlango na kuingia Ofisini humo,alimuona Bosi wake mpya.Macho yake bado yalikua kwenye kompyuta Yake ya mezani,huku akiendelea kumkaribisha mgeni wake na kumuelekeza akae kwenye kiti akiwa bado hajamtia machoni pake.

Aisha alikua tayari ameshamtazama vyakutosha na ametulia akiendelea kujidadisi kwa kujiangalia kila Mara kama kuna kasoro ambayo ingemkera bosi huyo asiyemjua,alikua ni kijana wa makamo ambae ni kama alimwacha Aisha kwa karibia miaka mitano kiumri, unadhifu wake ulizidi kuleta  uzuri wa ofisi Yake.

"Okey,Welcome nadhani naongea na Aisha mbele yangu bila Shaka,na... aaah Mimi naitwa Meshack Mbilwa ndiye msimamizi wa kampuni hii na utakua umeshafatilia inahusiana na biashara za namna gani,Chamsingi umeshafika nadhani nikukaribishe tena na pia jiskie upo Nyumbani,jiskie ni familia yetu ondoa ugeni ili uweze kwenda sawa na wafanyakazi uliowakuta hapa" Aliongea bwana Mbwila bila kituo cha hata kumpa nafasi Mgeni wake aongee.

Aliendelea na mazungumzo yake ya hapo Ofisini na mwisho kumchukua Aisha amfuate  kuanza kumtembeza kwenye ofisisi zote zilizopo hapo.

Baada ya kufanya utambulisho huo kwa wafanyakazi wote kwa Aisha na kwa upande wakwao, kilicho baki ilikua kumwonesha ofisi ambayo ndio maalumu kwa ajili ya Aisha.Ofisi za Kampuni hii zilikua katika mfumo wa kisasa japo haikua kampuni kubwa Lakini ilidizainiwa kwa mwonekano uliopendeza zaidi.Kutoka ofisi moja kwenda nyingine kulitengwa na kuta za vioo vigugumu vinavyoonesha nje na sio aliye nje aone ndani.

"Hii ndiyo ofisi yako Aisha,nikutakie majukumu Mema kazini endapo kutakua na tatizo lolote usisite kunishirikisha"

Bosi Mbilwa alionekana si muongeaji sana zaidi ya kufikisha kile alichotakiwa kisha aliondoka,Aisha alibaki na mshangao kwanini bosi hana hata muda zaidi ni mwenye haraka zaidi toka alipoonana nae.Hilo halikumuumiza kichwa kwani kila Mtu anahulka na silka yake.

Mpaka inafika alasiri ya siku hiyo,ni saa tisa na robo,ni muda wa kuondoka ulishafika,mlango wa Aisha uligongwa muda huo Aisha alikua akiendea na kazi zake hasa kukagua mafaili ambayo bado hayakufanyiwa kazi na yale ambayo kazi Yake haija kamilika.

"Ingia"

"Ooh Habari Dada Aisha,bado upo ofisini na muda umekwisha eti..."

Aisha alimkaribisha aliyepigahodi ambaye naye alimpokea kwa mvua ya maswali ya mshangao,kwanini bado yumo ndani na muda umeisha.Basi waliongea kitambo kidogo tu na Aisha alionekana kujitetea kuwa ameghafilika kuhusu kuondoka kutokana na kazi nyingi alizokutana nazo.

"Unaitwa Nani kwanza dadangu,mana tumeongea ila sjakujua mi mwenzio pale nimetambulishwa Majina yenu kwenye orientation ila sina nnalolikumbuka hapa"

"Hahahaaaa Da Aisha bhana acha kunchekesha,mi naitwa Rhoda mwaya ... hivi Dada ulikula kweli leo mana mpaka umesahau muda wa kuondoka"

"We acha tu kazi zipo nyingi, sijala yani"

"Basi sio swala hilo twende mana sio muda walinzi watakuja na ofisi itafungwa,tupite mgahawani tupate chakula eti,ama unawazo lingine Kipenzi"

Alikubali kisha wakapanda kwenye gari la Rhoda na kwenda kwenye mgahawa wa karibu na ofisi yao,mgahawani hapo paliitwa  KDB Sharbat&Food Restaurant.

"Hivi ilikuaje ukapata ajira hapa Aisha,hahahhh samahani Lakini kwa swali langu kama ..." Aliuliza huku akijikosha

"Hapana bila samahani ni sawa,unajua umekua rafiki yangu wa mapema sana hapa Ofisini,na nadhani hilo ni swali la kirafiki tu si kama kuna ubaya hivyo usiwe na wasi na hilo,na kupata ajira hapa wala sina cha kukwambia kingine zaidi ya bahati,maana hata interview sikufanyiwa yani,Mungu huyu"

Rhoda alishangaa aliposkia hakuna usaili uliopita kwa Aisha.

"Inamana wamempitisha hivihivi kweli kuna jambo nyuma ya hili si bure"Aliwaza pekeyake Rhoda.

Aisha alikua anaendelea Kula na kunywa huku Mwenzie akionekana kupunguza ule uchangamfu aliokua nao mwanzo.

Kiumri Rhoda akikua amemzidi Aisha karibia miaka mitatu tu Lakini kila Mara  alipendelea kumuita Aisha Dada,haikua mbaya kwa Aisha alikubali na Maisha yaliendelea,baada ya kumaliza kupata chakula Waliingia kwenye gari kisha waliondoka,ambapo getini walipishana na Gari lingine jeusi aina ya Range,hili ni Aisha pekee aliliona kwani lilipita kwenye geti la kuingilia mbali kidogo na lango la kutoka upande ambao yeye alikua amekaa na kingine aliona ishara tofauti kwenye lile gari,mtu aliyekaaa dirisha la upande wake alishusha kioo na kumuangaalia Aisha mpaka pale alipokua mbali na upeo wa macho yake,Lakini hakumtambua ni nani.Hili pia halikua na uwezo kufungua fikra za Aisha,alilipotezea.

Ile Range ilifika mpaka paking ikasimama kwa dakika kadhaa,ndani ya gari hili kuna mazungumzo yalikua yakiendelea 

" Haikupaswa iwe hivi,ni kwanini amejenga mazoea haraka na wafanyakazi,ndani ya siku moja,inaonekana ni Kasuku huyu binti"

"Kila kitu kitakua sawa Mr,nadhani kuwa na Subra tu"

Dakika kumi zilitosha maongezi ya watu Hawa wawili yalikamilika kisha gari liliondoshwa...

Safari ya kina Aisha ilikua na stori nyingi njiani wakiongea mengi sana na walifurahi pamoja .

" Rhoda nashukuru sana Kipenzi hapa ndo nyumbani karibu uwaone wazazi basi"

"Hapana nadhani siku nyingine itakua special kwaajili ya hili,Muda naona umesogea sana jioni inakaribia sasa"

"Mmmmh ...basi sawa naona Sababu zako zina mashiko pia,nikutakie usiku mwema rafiki yangu "

"Nawe pia Kipenzi changu"

Waliagana vizuri na wote walikua na furaha machoni mwao lakini nafsini mwa Rhoda ilikua tofauti kwani kipo kinachompa wasiwasi kwa ujio wa Rhoda pale Ofisini.

Safari yake ilikua ni pale alipotoka nusu saa iliyopita,KDB Sharbat&Food Restaurant, alifoka na kushuka kuelekea kwenye sehemu ya Meza za chakula akaangaza angaza kisha akaondoka.

Rhoda ni msichana mrembo,ameumbika haswa humvutia kila mwanaume rijali,rangi na macho yake ni moja ya kivutio machoni pa mwanaume yeyote Yule.

 Kilichompeleka hakukipata hivyo alirudi nyumbani kwake na kuingia chumbani akajitupa kitandani akiangalia silingbodi za chumba hiko huku feni likizunguka kwa spidi na ni wazi halikua limezimwa tokea usiku wa jana.Mawazo madogo madogo yalimchukua na kumpeleka kwenye usingizi wa ndoto zilizo pishana bila mpangilio... Ila yote ni mawazo tu hakuna uhalisia.

Muda huu Aisha amefika kwa wazazi wake ambao walifurahi kama kawaida yao na hapo sasa ndipo walihisi kuna chochote chenye faida juu ya kumsomesha mtoto wao huyo wa pekee na tena ni wakike.Wakiongea mengi kuhusu siku ya Kwanza kazini,wazazi walipata chakula cha usiku kisha nyumba Nzima ilikua kimya...wote walilala.

Saa Saba imetimia usiku huu, simu ya Rhoda ilikua ikiita mfululizo ikikata inaita tena,Mara hii ilimwamsha aliyepigiwa na kuiangalia kisha kuiacha mpaka ilipo acha akaizima kabisa.

___________________

Nani anampigia Rhoda,Kwanini Rhoda anawasiwasi juu ya ya ujio wa Aisha Ofisini,ni kina Nani kwenye Range na mazungumzo yao yanalenga nini.

Usikose sehemu ya Pili kwenye Simulizi hii mpya kabisa.... Usisahau Kukoment hapo chini tupate sehemu ya pili mapema.

Post a Comment

Previous Post Next Post